Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira January Makamba (Mb) alieleza kuwa nchi yetu inakabiliwa kwa kiasi kikubwa na hali ya kuenea kwa jangwa na ukame na kwamba takwimu zinaonyesha kuwa takribani asilimia sitini na moja (61%) ya eneo la nchi liko katika hatari ya kugeuka jangwa.
Waziri Makamba ameyaeleza hayo ofisini kwake Mjini Dodoma wakati akizungumza na wanahabari katika kuelekea kwenye maadhimisho ya siku ya Kupambana na Kuenea kwa Hali ya Jangwa na Ukame Duniani ambayo inaadhimishwa ulimwenguni kote kila ifikapo tarehe 17 Juni (Leo) ambapo kauli mbiu ya mwaka huu ni “Ardhi ni Makazi yetu Tuitunze kwa Manufaa ya baadaye” (‘Our Land, Our Home, Our Future’) yenye malengo ya kuhamasisha jamii kuitunza Ardhi kwa kuwa ndiyo makazi yetu hii ikiwa ni pamoja na kuongeza juhudi zaidi kwa ajili ya manufaa ya baadaye kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Waziri Makamba ameeleza mikoa ambayo imeathirika zaidi kuwa ni pamoja na Singida, Dodoma, Shinyanga, Manyara, Simiyu, Geita na baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Arusha ambapo tayari madhara mbalimbali ya kuenea kwa hali ya jangwa na ukame yameanza kuonekana ikiwa ni pamoja na kukauka kwa vyanzo vya maji katika maeneo mbalimbali, vifo vya mifugo na wanyama pori, upungufu wa mvua kutokana na ukataji wa miti kiholela na migogoro baina ya wafugaji na wakulima kutokana na kupungua kwa maeneo ya kilimo na malisho ya mifugo.
Ili kupambana na hali ya kuenea kwa jangwa na ukame Waziri Makamba mwenye dhamana ya Mazingira nchini ameeleza kuwa serikali imechukua hatua mbalimbali zikiwemo kuandaa taarifa ya hali ya kuenea kwa jangwa na ukame (Status of Land Degradation) ya mwaka 2014, Mpango kazi wa Kitaifa wa Kupambana na kuenea kwa hali ya jangwa na ukame (National Action Program to Combat Desertification) ya mwaka 2014-2018 lakini pia amesisitiza matumizi ya nishati mbadala ili kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa, kuendeleza njia bora kuhifadhi maji na uvunaji wa maji hasa kipindi cha mvua na kuelekeza wananchi kuwa na shughuli zingine za uzalishaji mali (Other income generating activities) ili kupunguza utegemezi katika maliasili.
Vilevile ameainisha uwepo wa programu ya kitaifa ya upandaji miti ya mwaka 2016 hadi 2021 ambayo inalenga kupanda miti zaidi ya milioni 280 huku ikilenga hasa maeneo yaliyo katika hatari za kukabiliwa na hali ya jangwa na ukame.

No comments:
Post a Comment